Wanaowaficha wagonjwa wa Ebola mashakani

Haki miliki ya picha AFP GETTY
Image caption Ebola

Bunge nchini Sierra Leone limepitisha sheria inayotoa hukumu ya miaka miwili jela kwa mtu yeyote atakayepatikana akimficha makusudi mtu aliyeambukizwa viini vya ugonjwa wa Ebola.

Afisa mmoja wa serikali anasema kuwa hatua hiyo inalenga kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa huo.

Wakati huohuo Ivory Coast imefunga mpaka wake na Liberia na Guinea.

Serikali ya Ivory Coast imesema kuwa hatua hiyo inatokana na ueneaji wa maambukizi ya ugonjwa huo katika mataifa hayo jirani.

Ni taifa la hivi karibuni barani Afrika kuweka vikwazo vya usafiri licha ya onyo kutoka kwa shirika la afya duniani kwamba hatua hiyo huenda ikasababisha uhaba wa chakula katika mataifa yalioathiriwa.