Kenya kupambana na wafanyakazi ghushi

Image caption Mfumo mpya unalenga kupambana na wafanyakazi bandia wanaopokea mishahara bila kufanya kazi

Maafisa wakuu nchini Kenya wamezindua mpango mpya wa kuwasajili wafanyakazi wa serikali kwa njia ya kielektroniki, ili kukabiliana na wafanyakazi ghushi wanaokula mishahara bila ya kufanya kazi.

Serikali inasema kuwa maelfu ya wafanyakazi wa umma waliostaafu huendelea kupokea mishahara kwa njia ya udanganyifu.

Jambo hilo hugharimu serikali ya Kenya mamilioni ya dola kila mwezi kwa malipo yasiyostahili.

Taarifa ya serikali imesema kuwa wafanyakazi wa umma wanahitajika kujisajili kielektroniki katika kipindi cha wiki mbili zijazo, au hawatapokea misharaha yao.

Rais Uhuru Kenyatta aliahidi kupambana na rushwa katika sekta ya umma baada ya kuchukua usukani mwaka 2013.

Serikali ya kenya inaamini kuwa maelfu ya watu hudai kulipwa mishahara kwa njia ya udanganyifu swala linaloigharimu serikali takriban dola millioni 20 kwa mwaka.

katika visa vyengine wafanyikazi hupokea zaidi ya mshahara mmoja huku wafanyakazi waliokufa pia wakidaiwa kupokea mishahara.

Tatizo la wafanyikazi ghushi ni swala la kawaida katika mataifa mengi ya bara afrika.

Nigeria ilianzisha mfumo wa vitambulisho vya kielektroniki wiki iliopita ili kukabiliana na swala hilo huku Ghana na Senegal zikidaiwa kuanzisho mifumo kama hiyo.