Viongozi wa AU wajadili usalama Kenya

Image caption Swala la ugaidi katika mataifa ya Afriak mashariki limetokana na Somalia kukosa uthabiti

Viongozi wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika wanakutana mjini Nairobi,nchini Kenya katika mkutano unaoanza leo.

Viongozi hao wanatarajiwa kujadili masula yanayohusu nchi wanachama hasa masuala ya ugaidi, matumizi ya nguvu kupitiliza na matarajio ya baadaye ya nchi wanachama wa umoja huo.

Mkutano kama huo uliofanyika Equatorial Guinea ukijadili masuala ya vitisho kuhusiana na ugaidi na kuainisha kwamba yameathiri amani na uchumi wa nchi nyingi barani Afrika.

Marais kutoka nchi wanachama wa AU tayari wanahudhuria mkutano huo ambao utalipa kipaombele swala la ugaidi na tisho la ugaidi ambalo bado ni kizungumkuti kwa mataifa ya Afrika hasa Afrika Mashariki na mataifa ya upembe mwa Afrika.

Mkutano huo unalenga kuafikia hatua mwafaka za kupiga jeki juhudi zinazofanywa dhidi ya ugaidi ikiwemo kuwianisha sheria za kimataifa kuhusiana na ugaidi.

Kadhalika viongozi wanatafuta nyenzo za kupata msadaa zaidi katika ushirikiano wa kimataifa kupambana na ugaidi.

Viongozi wanaohudhuria mkutano huo ikiwemo marais wa Uganda, Tanzania, Chad, Niger, Nigeria,Somalia pamoja na mawaziri wakuu wa Namibia, Algeria na naibu rais wa Burundi wanatarajiwa kukubaliana kuhusu kuimarisha hatua za kupambana na ugaidi kitaifa, kikanda na kimataifa.

Mkutano huu unafanyika wakati mataifa ya kiafrika yakipambana na swala la itikadi kali za kidini ambazo zimezagaa miongoni mwa wananchi wa mataifa hayo.