Nyumba ya Big Brother yateketea A.Kusini

Image caption Cherise Makubale wa Zambia ndiye alikuwa mshindi wa kwanza wa Big Brother

Uzinduzi wa makala mapya ya kipindi maarufu cha Big Brother nchini Afrika Kusini umeahirishwa baada ya moto mkubwa kuteketeza studio za kipindi hicho mjini Johannesburg.

Kipindi hicho kilistahili kuanza Jumapili hii lakini waandaaji wa wa kipindi chenyewe wameamua kuahirisha uzinduzi huku wakitafuta sehemu nyingine ya kupeperushia kipindi hicho.

Hakuna aliyejeruhiwa kwenye mkasa huo wa moto na kilichousababisha bado hakijajulikana kwani uchunguzi untarajiwa kufanywa.

Washiriki katika kipindi hicho kutoka nchi 14 Afrika watakuwa wanashiriki katika makala ya 9 ya kipindi hicho.

Kipindi chenyewe kinatarajiwa kupeperushwa kwa siku 99 kabla ya mshindi kutangazwa.

Mshindi wa mwaka huu anatarajiwa kupokea kitita cha dola 300,000 kima sawa na kile kilichotolewa kwa mshindi mwaka 2013.

Waandalizi wa kipindi hicho Endemol na M-Net walisema kuwa juhudi za kupata sehemu mbadala ya kuendeshea kipindi hicho itakuwa kazi ngumu kutokana na ukosefu wa teknolojia inayohitajika kuendeshea kipindi hicho kwani haipatikani kwa urahisi.

''Kila juhudi italenga kupata ufumbuzi haraka iwezekanavyo kuhakikisha kuwa kipindi hicho ambacho hutazamwa na watu wengi zaidi Afrika kitaendelea.''waliongeza kusema waandalizi.

Waandalizi pia walisema kuwa washiriki kutoka Ghana walipata tatizo la viza na hivyo wakaamua kuchua raia wa Ghana wanaoishi nchini Afrika Kusini kwenyewe.

Pia washiriki wapya walitarajiwa kutoka Rwanda na Sierra Leone kwa mara ya kwanza lakini kutokana na changamoto za hapa na pale hawataweza kushiriki.

Kipindi cha Big Brother ni kipindi maarufu sana Afrika kutokana na kupendwa sana kwake, na kilianza kupeperushwa mwaka 2003. Washiriki kutoka Tanzania, Angola, Nigeria, Namibia, Zimbabwe na Afrika Kusini wamewahi kushinda katika makala ya awali.

Mnamo mwaka 2010, kipindi hicho kiligonga vyombo vya habari baada ya mshiriki mmoja kutimuliwa kutoka katika nyumba hiyo baada ya kumpiga makonde mshindani mwanamke.