Ebola:Zaidi ya watu 1900 wamefariki

Image caption dawa dhidi ya Ebola

Zaidi ya watu 1,900 wanakisiwa kufariki kutokana na mlipuko wa Ebola katika kanda ya Afrika Magharibi.

Taarifa hii ni kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO.

Visa 3,500 vimethibitishwa vya wagonjwa wa Ebola, kuambukizwa ugonjwa huo nchini Guinea, Sierra Leone na Liberia.

''Inakuwa vigumu kudhibiti ugonjwa huo katika mataifa haya, '' alisema mkuu wa shirika hilo Margaret Chan.

Shirika hilo limeandaa mkutano wa siku mbili unaoanza leo Geneva Uswizwi ukilenga kujadili uwezekano wa matibabu dhidi ya ugonjwa wa Ebola.

Wataalamu, madaktari , watafiti na wadau wengine kutoka nchi zilizoathirika kutokana na ugonjwa huo, watahudhuria mkutano huo.

Shirika hilo linasema kuwa linahitaji zaidi ya dola milioni miatatu kupambana na ugonjwa huo na huenda watu elfu 20 wameathirika.

Dawa zote zenye uwezekano wa kutibu ugonjwa huo zitajadiliwa na kufanyiwa uchunguzi wa kina wa maoni ya kitaalam.

Hata hivyo shirika la misaada la dawa MSF limeonya kuwa huenda mkutano huo ukashindwa kuwa na matokeo makubwa katika mlipuko wa ugonjwa wa Ebola Afrika Magharibi ambako watu 1900 wamefariki kutokana na ugonjwa huo.

Mkuu wa shirika hilo la MSF Brice de la Vigne akikosoa kuhusiana na mkutano huo amesema kuwa kilichopaswa kutiliwa mkazo kwa sasa na mashirika ya kimataifa ni kuongeza idadi ya hospitali dharula katika maeneo ya milipuko ya Ebola.