Wezi wa gari la Rais Kenya mahakamani

Image caption Gari la msafara wa Rais Kenyatta lilipatikana mjini Kampala Uganda

Watu watano akiwemo raia mmoja wa Uganda pamoja na fundi mmoja wa magari wameshitakiwa kwa kosa la wizi wa gari la msafara wa ulinzi wa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta nchini Kenya.

Watano hao pia walishitakiwa kwa kumuibia gari inspekta wa polisi David Machui aliyekuwa akiendesha gari hilo aina ya BMW 735 tarehe 26 mwezi Agosti mjini Nairobi lilipoibwa.

Washukiwa hao wote walikanusha madai hayo kwamba walihusika katika wizi wa gari hilo.

Kila mshukiwa aliachiliwa kwa kima cha shilingi milioni 5 isipokuwa mwanamume mmoja aliyesemekana kuwa na kesi tofauti mahakamani.

Raia wa Uganda Robert Mande Ochan, aliamrishwa na mahakama kutoa dhamana ya shilingi milioni mbili ili aweze kuachiliwa.

Gari hilo lilipatikana mjini Kampala Uganda na kurejeshwa nchini Kenya siku ya Ijumaa.

Washukiwa hao walioiba gari hilo wakiwa wamejihami, wanashukiwa kuwa sehemu ya mtandao wa wezi wa magari wakiendeshea kazi yao nchini Kenya, Burundi, DRC , Tanzania na Uganda.

Kikundi hicho kiko na wahalifu, maafisa wafisadi wa kutoza ushuru na mafundi wa magari.

Polisiwa wa Uganda walipata hari hilo baada ya mpenzi wa mshukiwa mmoja kumuwekea mtego ambao ulimfikisha kwa polisi, katika mtaa wa Wandegeya, mjini Kampala.

Maswali yamekuwa yakiulizwa kuhusu ambavyo afisaa wa polisi aliruhusiwa kuendesha gari la serikali kama gari lake binafsi, wakati ambapo utaratibu unasema kuwa magari yote ya serikali yanapaswa kuegeshwa katika kituo cha polisi kilicho karibu na dereva wa gari hilo.