Ebola inaenea kwa kasi nchini Liberia

Haki miliki ya picha PA
Image caption Shirika la afya duniani linataka juhudi kuongezwa katika vita dhidi ya Ebola

Ugonjwa wa Ebola unaenea kwa kasi nchini Liberia huku maelfu ya watu wakiambukizwa upya na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka katika muda wa wiki tatu zijazo.

Hii ni kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO.

Shirika hilo linasema kuwa njia zinazotumika kukabiliana na janga la Ebola hazijafanikisha vita dhidi ya Ebola.

Takriban watu 2,100 wamefariki kutokana na ugonjwa huo katika kanda ya Afrika Magharibi hasa katika mataifa ya Guinea, Liberia, Sierra Leone na Nigeria mwaka huu.

Kwa mujibu wa shirika hilo wahudumu 79 wa afya pia wamefariki kutokana na ugonjwa huo.

Kadhalika shirika hilo limesema kuwa, mashirika yanayopambana na mlipuko wa ugonjwa huo, yanahitajika kuongeza juhudi.

Wakati huohuo , shirika la madaktari wasio na mipaka la Medecins Sans Frontieres linasema kuwa limelemewa kabisa na idadi inayozidi kuongezeka ya wagonjwa wa Ebola nchini Liberia.

Shirika hilo linasema kuwa kituo chake cha kutoa matibabu mjini Monrovia huwarudisha nyumbani watu wanaohitaji matibabu kila siku .

Msemaji wa shirika hilo Sophie Jane Madden aliambia BBC kuwa hali hiyo sasa ni ya vurugu na isiyodhibitika ambapo ametoa wito wa msaada wa kimataifa.

Mapema shirika la afya duniani WHO lilionya kuwa Liberia huenda ikashuhudia maelfu ya visa vya maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ebola majuma yanayokuja.

Watu 1000 tayari wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo kwenye taifa hilo la Afrika Magharibi.