Seneta wa zamani wa Rwanda apata afueni

Image caption Mafuvu ya waathiri wa mauaji ya kimbari Rwanda

Seneta wa zamani nchini Rwanda aliyeshitakiwa makosa ya mauaji ya kimbari Anastase Nzi-ra-sa-na-ho ameshinda kesi yake ya rufaa.

Mahakama ya rufaa mjini Kigali imebatilisha hukumu iliyokuwa imetolewa awali ya kifungo cha maisha jela mtu akifungiwa katika chumba chake kidogo.

Seneta huyo ni miongoni mwa wanasiasa wachache nchini humo walioshinda kesi zao baada ya kushitakiwa makosa ya mauaji ya kimbari. Ifwatayo ni taarifa ya mwandishi wa BBC Yves Bucyana.

Mama huyu akiangua kilio kinachojaa furaha akisema “mungu asifiwe …Mungu ndiye mkubwa,najawa na furaha isiyo kifani” hii ni baada ya jaji wa mahakama ya rufaa kutangaza kuwa seneta huyo ameshinda kesi yake.

Jaji amesema kwamba Seneta Nzirasanaho hana hatia ya kumiliki silaha kinyume cha sheria,silaha ambazo katika kesi ya awali zilitangazwa kuwa alizigawa kwa wanamgambo wa Interahamwe zikatumiwa kuua watu wa kabila la watutsi.

Jaji amesema hoja za mwendesha mashitaka hazikuweza kuishawishi mahakama ya rufaa kuthibitisha kuwa seneta huyo ana hatia.Aidha imetangazwa kwamba upande wa mashitaka haukuweza kuleta ushahidi wa kutosha kwamba Nzirasanaho mwenyewe aligawa silaha kwa wanamugambo.

Katika mahakama ya awali yeye mwenyewe alikuwa amekiri kuwa wakati wa mauaji ya kimbari akiwa anaendesha gari lake aliombwa na askari mmoja aliyesheheni silaha kumsafirisha hadi katika kijiji chake asilia lakini kwamba hakujua silaha hizo zitakavyotumiwa. Hoja yake nyingine ikiwa kwamba kesi ilipambwa kutokana na chuki za kisiasa kutoka kwa baadhi ya wanasiasa waliokuwa katika chama kimoja cha Social democratic.

Wahusika wote katika kesi hii ,iwe upande wa mshtakiwa au upande wa mashitaka hakuna hata mmoja aliyehudhuria kesi hii.Bado kuna fursa ya kukata rufaa katika mahakama kuu ikiwa kuna upande usioridhia uamuzi huo.

Bwana Nzirasanaho alihudumu kama seneta kwa kipindi cha miaka 8 tangu mwaka 2003 hadi mwisho wa muhula wake mwaka 2011.

Hadi kufikia sasa amekuwa miongoni mwa wanasiasa wachache walioshinda kesi za makosa ya mauaji ya kimbari ya Rwanda.