Ebola:Jeshi la Marekani kusaidia Liberia

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Liberia imeathirika sana na mlipuko wa Ebola

Rais wa Marekani Barrack Obama hii leo anatazamiwa kutangaza mpango wake wa kuwatuma wanajeshi 3,000 nchini Liberia kama njia moja ya kusaidia katika vita dhidi ya ugonjwa hatari wa Ebola.

Wanajeshi hao watasimamia ujenzi wa vituo vipya vya kimatibabu na pia watahusika katika utoaji wa mafunzo ya kimatibabu kwa wahudumu.

Kumekuwa na malalamishi kwamba jamii ya kimataifa imelegea katika harakati za kukabiliana na mkurupuko wa Ebole katika mataifa ya Afrika magharibi.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Wanajeshi hao watatumika kuunda muundo msingi wa kupamabana na Ebola Liberia

Mataifa ya Sierra Leone, Liberia na Guinea ndiyo yaliyoathirika zaidi huku zaidi ya watu 2,400 wakiwa tayari wamepoteza maisha yao kufikia sasa.

Zaidi ya nusu ya idadi ya watu waliofariki kutokana na ugonjwa huu ni raia wa Liberia.

Shirika la afya duniani (WHO) limetahadharisha kuwa huenda watu zaidi wakazidi kufariki.

Umoja wa Mataifa (UN) unapangiwa kuzungumzia jinsi ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika mkutano unaopangiwa kufanyika huko Geneva.

Kulingana na viongozi nchini Marekani, mpango wao wa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola unalenga-:

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Zaidi watu 2400 wameaga dunia kutokana na Ebola

Utoaji wa mafunzo ya kimatibabu kwa wahudumu wa kiafya 500 kila juma.

Ujenzi wa vituo vya matibabu 17, kila chumba kikiwa na vitanda kumi.

Usambazaji wa vifaa vya huduma ya afya kwa kila nyumbaKampeni ya kuwahamasisha wananchi kuhusu jinsi ya kuwashughulikia wagonjwa wa Ebola.

Ujenzi wa kituo cha kijeshi cha pamoja mjini Monrovia kitakachotumiwa katika shughuli ya kupokea msaada kutoka kwa jamii ya kimataifa.

Wadadisi wa masuala ya kimatibabu wamepongeza mpango huu wa Marekani huku wengine wakitilia shaka nia ya Marekani nchini Liberia.