Wahamiaji kutoka Libya wazama baharini

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wahamiaji wengi wamekufa maji wakitokea LIbya

Wahamiaji wengi kutoka Libya wameripotiwa kupoteza maisha yao baada ya mashua waliyokuwa wakisafiria kuzama ikielekea upande wa Italia.

Kwa mujibu wa wanajeshi wa majini wa Libya, watu hao walikuwa wakijaribu kuvuka kuelekea Ulaya.

Msemaji wa majeshi ya majini ya Libya, Ayub Qassem amethibitisha watu 36 wameokolewa baada ya mashua yao iliyokuwa imebeba watu 250 ilipozama karibu na eneo la Tajoura, mashariki mwa Tripoli.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Asilimia kubwa ya wahasiriwa ni wanawake na watoto

Hata hivyo, amefichua ya kwamba maiti nyingi bado zinaelea baharini.

Mkasa huu umetokea wiki chache tu baada ya mashua nyingine tatu kuzama mfululizo katika njia ya baharini inayotoka Libya hadi Italia.

Kumekuwa na ongezeko la watu wanaoikimbia nchi ya Libya mwaka huu kutoka na ghasia zinazoshuhudiwa, huku walunguzi wa binadamu wakipata fursa ya kutekeleza uhalifu wao.

Waasi wamekuwa wakipigania udhibiti wa miji na vituo muhimu nchini Libya.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Makundi hasimu ya waasi wamekuwa wakipigana wakijaribu kutawala sehemu kubwa ya taifa hilo

Wanajeshi wa majini wa Libya wamelalamikia ukosefu wa vifaa na uwezo wa kutosha wa kukabiliana na mikasa.

Wamedai imewabidi kuazima mashua kutoka kwa wavuvi na kampuni nyingine.

Bw. Qassem amefafanua ya kwamba wengi wa wahamiaji hao walikuwa waafrika na pia jinsia ya kike.