Vyombo vya habari,usalama vyakutana TZ

Image caption Katibu wa Baraza la Habari Tanzania, Kajubi Mukajanga

Uhasama wa kiutendaji kati ya vyombo vya habari na vya ulinzi na usalama nchini Tanzania huenda ukapungua kwa kiasi kubwa baada ya pande hizo kuanza kukaa pamoja na kujadili mambo yanayokwamisha utekelezaji wa majukumu yao.

Baraza la Habari Tanzania limeitisha mkutano wa mashauriano kati ya vyombo vya habari na vyombo vya ulinzi, usalama na sheria ili kutambua kazi, haki na wajibu wa kila upande kwa maslahi ya umma.

Kila upande umekuwa ukitetea kuwa unatekeleza majukumu yake kwa maslahi ya umma. Hata hivyo vyombo vya habari ndivyo ambavyo vimeelekeza lawama zaidi kwa vyombo vya ulinzi na usalama kuwa vinakandamiza uhuru wa vyombo vya habari kupata na kutoa taarifa zenye maslahi kwa umma.

Kwa upande wake vyombo vya ulinzi na usalama vimekuwa vikivilaumu vyombo vya habari kwa kutoa habari na hata kulazimisha kutoa habari zinazohatarisha usalama wa umma.

Akizungumza katika mkutano huo Makamu wa Rais wa Tanzania Dokta Gharib Bilal amesema katika ulimwengu wa sasa suala la habari limetanuka kiasi kwamba sheria zilizopo kusimamia vyombo vya habari hazina budi kuangaliwa upya ili kukidhi mazingira ya sasa.

“Si rahisi tena kudhibiti mawasiliano ama taarifa kwa kutumia sharia tulizojiwekea kama nchi maana jambo linaweza kudhibitiwa nchi moja na kutangazwa nchi nyingine na likarejea kule kule lilikodhibitiwa.” Amesema.

Hata hivyo Dokta Bilal amesema kuna umuhimu wa kuangalia mbinu za kukabiliana na mawasiliano yenye kuhatarisha usalama wa umma.

Amesema vyombo vya habari na vyombo vya usalama vina mipaka ya utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Dokta Bilal amesema mikwaruzano ya vyombo hivi inatokana na chombo kimoja kutaka kupata habari hata katika mazingira ambayo vyombo vya usalama vinaona ni hatari.

Kwa upande wake katibu mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania Mukajubi Mukajanga amesema,”vyombo vya usalama na sheria na vyombo vya habari vina uhusiano wa mashaka.Kuna wakati ambao wanadhani wanahitajiana wanakuja pamoja na kuna wakati ambapo kuna uhasama mpaka watu wanapigwa….”

Bwana Mukajanga amesema kutokana na umuhimu wa vyombo hivi kushirikiana katika masuala mbalimbali ya kijamii, baraza lake likaamua kuwakutanisha pamoja ili kujenga moyo wa kuaminiana.

Baraza la Habari Tanzania limewakutanisha waandishi wa habari na vyombo vya ulinzi na usalama ili kujadili mambo yanayokwamisha utekelezaji wa majukumu yao.