Obama:'Ebola ni tisho kwa usalama'

Haki miliki ya picha AP
Image caption Rais Barack amezitaka nchi zengine kutoa msaada wao katika kupambana na Ebola

Rais wa Marekani Barack Obama, amelitaja janga la Ebola katika kanda ya Afrika Magharibi kuwa tisho la usalama wa kimataifa.

Obama ametoa kauli hiyo huku akitangaza jukumu la Marekani katika kupambana na janga la Ebola.

''Dunia nzima inaelekeza macho ya kutaka msaada kwa Marekani,'' alisema Rais Obama, lakini akaongeza kwamba mlipuko unaoshuhudiwa wa janga hilo, unahitaji kushughulikiwa na jamii ya kimataifa.

Hatua ambazo Marekani imetangaza ikiwemo kupeleka wanajeshi 3,000 katika kanda hiyo kupambana na Ebola na kujenga taasisi za afya.

Ugonjwa wa Ebola umewaua watu 2,461 mwaka huu, kulingana na shirika la afya duniani (WHO).

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Utafiti wa chanjo ya Ebola

Tangazo hilo limetolewa huku Maafisa wa Umoja wa Mataifa wakitaja ugonjwa huo kuwa janga la kimataifa na pia janga kubwa kushuhudiwa kwatika miaka ya hivio karibuni.

Pesa za msaada zinazohitajika kupambana na Ebola zimeongezeka mara kumi katika mwezi mmoja uliopita na kwamba dola bilioni ndizo zinahitajika kukabiliana na ugonjwa huo.

Hii ni kwa mujibu wa mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ebola.

Rais Obama amezitaka nchi zingine kuongeza kasi ya kusaidia katika vita dhidi ya Ebola kwani kukithiri na kuendelea kuenea kwa ugonjwa huo kutasababisha changamoto za kiuchumi , kiusalama na kisiasa.