Scotland yakataa kujitenga

Raia wa Uingereza wakisherekea ushindi
Maelezo ya picha,

Raia wa Uingereza wakisherekea ushindi

Scotland imefanya uamuzi wa mwisho kuwa itaendelea kubakia kama sehemu ya Uingereza , raia kwa pamoja wamekataa uhuru wa Scotland.

Kundi linalotaka kuendelea kuwa chini ya Himaya ya Uingereza inayojiita, Better Together, ilishinda kwa karibu nukta 10 asilimia.

Kundi hili lilipata kura nyingi katika maeneo ambayo awali ilidhaniwa wanaotaka kujitenga wangepata ushindi.

Kiongozi wa Better Together, Alistair Darling, alisema wakazi wa Scotland wamechagua mabadiliko ya manufaa badala ya kutengana kusiko na maana.

Maelezo ya picha,

Raia wa Scotland wamepiga kura kusalia sehemu ya Uingereza

Kiongozi wa kundi lililotaka kujitenga, Alex Salmond, alikubali kushindwa lakini akasisitiza kuwa siku za usoni kungali kuna uwezekano wa eneo hilo kujitenga.

Lakini Waziri Mkuu David Cameron amesema kuwa wananchi wamefanya uamuzi wa kizazi kizima.

Alisema amefurahishwa na matokeo hayo.

Alimteua Lord Smith of Kelvin kusimamia shughuli za mabadiliko maalumu yanayopaswa kufanywa ili Scotland iweze kujifanya maamuzi yake mengine kwa njia ya uhuru.

Maelezo ya picha,

Kura zikihesabiwa

Wapiga kura 2,001,926 walipiga kura kusalia kama sehemu ya Uingereza huku wapiga kura 1,617,989 wakipiga kura kujitenga .

Ushindi huo ni asilimia 55 dhidi ya 44 waliokuwa wakiunga mkono hatua ya kujitenga.

Waziri Kiongozi wa Scotland Alex Salmond amesema ameridhia kuanguka katika mchakato wa kura ya maoni.