Ebola:Amri ya kutotoka nje yatekelezwa

Serikali ya Sierra imetoa amri ya kutotoka nje kwa siku tatu.
Maelezo ya picha,

Serikali ya Sierra imetoa amri ya kutotoka nje kwa siku tatu.

Serikali ya Sierra imetoa amri ya kutotoka nje kwa siku tatu.

Lengo la amri hii ni kuhakikisha kuwa kila mtu amekaa nyumbani huku wahudumu wa afya wakiendelea kuwatafuta wagonjwa kwa lengo la kuwaweka karantini ili kuzuia kuenea zaidi kwa Ebola.

Hata hivyo, wakosoaji wamesema amri hiyo itaharibu uhusiano kati ya madaktari na wananchi.

Nchi ya Sierra Leone ni moja kati ya nchi za Afrika Magharibi zilizoathirika sana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola huku zaidi ya watu 2,600 wakipoteza maisha yao.

Alhamisi, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa (UN) lilitangaza kuwa mlipuko huo ni tishio kwa usalama na amani duniani.

Baraza hilo liliomba mataifa yote kusadia katika harakati za kukabiliana na ugonjwa wa Ebola.

Maelezo ya picha,

Serikali inapania kutumia muda huo kuwatibu wagonjwa

Mvua kubwa iliyoshuhudiwa mjini Freetown hapo Alhamisi haikuwazuia maelfu ya wananchi wa Sierra Leone kwenda sokoni na pia katika maduka ya jumla kununua vyakula vya kutosha kabla ya amri ya kutotoka nje iliyotangazwa na rais kuanza kutekelezwa.

Serikali ya Sierra Leone inaanimi hatua hii itasaidia pakubwa katika harakati za kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa Ebola ambao umeathiri wilaya 13 kati ya wilaya 14 zilizo nchini humo na kusababisha watu zaidi ya 500 kupoteza maisha yao.

Shirika la madaktari wasio na mipaka wa Medecin Sans Frontieres wamekuwa wakipinga hatua ya kutoa amri ya kutotoka nje, wakisema hatua hiyo itachangia kusambaa kwa ugonjwa huo.

Maelezo ya picha,

Maduka mengi yamebakia yamefungwa

Mwezi uliopita, taarifa kutoka Shirika hilo ambalo wafanyakazi wake wamekuwa wakisaidia katika harakati za kukabiliana na mkurupuko huo, ilisema karatini na amri ya kutotoka nje itasababisha hali ya kutoaminiana kati ya wahudumu wa afya na wananchi nchini humo na kuwafanya wengi kuficha hali zao za kiafya.

Hata hivyo mamlaka nchini humo imesisitiza kwamba hatua hiyo yao itasaidia kupunguza kasi ya kuenea kwa ugonjwa huo na kuongeza kwamba watawatuma baadhi ya viongozi kuhakikisha watu hawatoki katika nyumba zao.