Lampard ainusuru Man City 1-1 Chelsea

Lampard ainusuru Man City 1-1 Chelsea
Maelezo ya picha,

Lampard ainusuru Man City 1-1 Chelsea

Mfungaji wa mabao mengi zaidi wa Chelsea Frank Lampard aliingia uwanjani kuiwakilisha Manchester City na akaisaidia kunusuru hadhi yake mbele ya vinara wa ligi hiyo Chelsea uwanjani Etihad .

Lampard - ambaye anaichezea City kwa mkopo kutoka New York City FC hadi Januari mwakani anajivunia taji la kuifungia Chelsea mabao 211 katika mechi 648 leo alifunga bao lake la kwanza dhidi yake .

Hata hivyo dakika tano alizoingia uwanjani kama mchezaji wa akiba zilitosha kumsaidia kusawazisha bao la Andre Schurrle ambalo lilikuwa limeiweka the Blues alama nane zaidi ya mabingwa hao watetezi wa ligi kuu ya Uingereza baada ya mechi tano .

Vijana wa Manuel Pellegrini walikuwa na mlima wa kupanda haswa baada ya kumpoteza kiungo wao Pablo Zabaleta.

Zabaleta alioneshwa kadi yake ya pili ya njano baada ya kumchezea visivyo mshambulizi machachari wa Chelsea Diego Costa.

Umati wa mashabiki wa Chelsea ulimshabikia Lampard licha ya kuwa ndiye iliyetia kitumbu chao mchanga dhidi ya wapinzani wao.

Licha ya sare hiyo vijana wa Jose Mourinho wamesalia na alama tatu kileleni mwa jedwali la ligi kuu ya Uingereza .

Kufuatia matokeo hayo The Blues walipoteza rekodi yao ya kushinda kila mechi na watajilaumu wenyewe kwa kupoteza alama 2 muhimu dhidi ya timu iliyokuwa na wachezaji 10 katika dakika 5 za mwisho.

Mechi hiyo ilisalia sare tasa kwa asilimia kubwa baada ya Kocha Manuel kumtuma mlinzi wake wa kutegemewa Vincent Kompany kumdhibiti Diego Costa kazi aliyoitekeleza kwa ukakamavu na kumnyima mhispania huyo nafasi ya kuongeza idadi ya mabao zaidi ya 7 alizofunga tayari katika mechi 4 alizoshiriki msimu huu.

Kompany akishirikiana na mlinzi mpya Eliaquim Mangala, aliyetokea Porto,kwa gharama ya pauni milioni 32 walifaulu kumdhibiti Costa.

Sare hiyo ilifuatia matokeo mengine ya kushngaza ambapo Manchester united ilipoteza udhibiti wa mechi yake dhidi ya Leicester ilipokuwa ikiongoza mabao 3-1 na ikambulia kichapo cha mabao 5-3.

Maelezo ya picha,

Kipa wa United David de Gea akikosa bao la 5 dhidi ya Leicester

Manchester United ilikuwa inaongoza mabao 2-1 kufikia muda wa mapumziko.

Kocha Louis van Gaal atalazimika kufanya muujiza ilikuimarisha safu yake ya ulinzi kwani kwa sasa huo ndio upungufu wake mkubwa .

Isitoshe van Gaal hana budi kutafuta mlinzi atakayeziba pengo lilioachwa na Tyler Blackett ambaye alionyeshwa kadi nyekundu atakaokutana na West Ham katika mechi yake ijayo.

Masaibu yake hayajaishia hapo ,Mreno huyo anasubiri kujua hatima ya mlinzi wake Jonny Evans aliyejeruhiwa na hivyo anasubiri kauli ya madaktari.