Uturuki yafunga baadhi ya mipaka

Wakimbizi kutoka jamii ya wakurdi ikivuka mpaka kuingia Uturuki kutoka Syria
Maelezo ya picha,

Wakimbizi kutoka jamii ya wakurdi ikivuka mpaka kuingia Uturuki kutoka Syria

Mamlaka nchini Uturuki zimefunga baadhi ya mipaka yake na nchi ya Syria kwa mara nyingine baada ya takriban watu elfu sabini wa jamii ya kikurdi kutoka nchini Syria kuingia nchini humo.

Inaarifiwa wakimbizi hao wanawakimbia wanamgambo wa kundi la Islamic State.

Siku ya Jumapili mapigano yalizuka kati ya vikosi vya usalama vya Uturuki na wapiganaji wa kikurdi waliokuwa wamekusanyika katika eneo la mpaka wakiwatafuta ndugu zao miongoni mwa wakimbizi.

Jamii nyingine ya kikurdi ilijaribu kuvuka hadi nchini Syria ili kujiunga na wanamgambo ambao wanaelezwa kuwa wameukaribia mji wa Kobani.

Wapiganaji wa IS wameteka sehemu kubwa ya Iraq na Syria katika miezi ya hivi karibuni.

Tayari kuna wakimbizi zaidi ya milioni moja wa Syria nchini Uturuki.

Wamekuwa wakitoroka tangu kuanza kwa mapambano dhidi ya serikali ya Rais Bashar al-Assad miaka mitatu iliyopita.

Baadhi ya wakimbizi wageni,wanapata hifadhi katika majengo ya shule ambayo yamesongmana watu huku Uturuki ikikabiliana na idadi kubwa na wakimbizi wanaoendelea kuingia nchini humo.