Mhubiri Abu Qatada aachiliwa huru

Abnu Qatada alikabiliwa na tuhuma za kupanga njama ya mashambulizi ya kigaidi nchini Jordan
Maelezo ya picha,

Abnu Qatada alikabiliwa na tuhuma za kupanga njama ya mashambulizi ya kigaidi nchini Jordan

Mhubiri muisilamu mwenye utata ambaye alihamishwa kutoka Uingereza mwaka 2013, Abu Qatada, ameachiliwa huru nchini Jordan baada ya mahakama kutompata na hatia.

Alikuwa ametuhumiwa na kosa la kuhusika katika njama ya kupanga mashambulizi ya kigaidi ambayo ilitibuliwa mwaka 2000.

Jopo la majaji waliokuwa katika mahakama hiyo, hawakumpata na hatia yoyote bwana Qatada kutokana na madai kuwa alihusika na njama hiyo ya ugaidi.

Uamuzi huo umetolewa baada ya Abu Qatada kutopatikana na hatia mwezi Juni katika kosa lengine la kupanga njama ya mashambulizi mwaka 1998 nchini Jordan.

Abu Qatada alitimuliwa kutoka Uingereza mwezi Julai mwaka 2013 kwa madai ya kueneza itikadi kali Uingereza ikitaka afunguliwe mashitaka nchini Jordan.