Balozi wa zamani Vatican matatani

Balozi Dominica Jozef Wesolowski anadaiwa kuwalawiti watoto wavulana katika Jamhuri ya Dominica
Maelezo ya picha,

Balozi Dominica Jozef Wesolowski anadaiwa kuwalawiti watoto wavulana katika Jamhuri ya Dominica

Vatican imempa kifungo cha nyumbani aliyekuwa balozi wake katika jamuhuri ya Dominica Jozef Wesolowski.

Inaarifiwa hatua hiyo imechukuliwa dhidi ya balozi huyo wa zamani kwa kosa la kuwadhalilisha watoto kijinsia.

Kasisi huyo wa zamani aliondolewa wadhifa wake mwezi Juni baada ya jopo la viongozi wa kanisa kumpata na hatia ya kuwalawiti watoto wavulana wakati akifanya kazi katika Jamuhuri ya Dominica.

Kesi yake itasikilizwa na mahakama ya uhalifu ya Vatican. Itakuwa kesi ya kwanza kumhusisha afisa wa ngazi ya juu kusikilizwa katika mahakama hiyo.

Wesolowski, ambaye asili yake ni kutoka Poland, alihudumu kama balozi wa Papa katika jamuhuri hiyo kwa kipindi cha miaka mitano.

Msemaji wa Vatican, alisema kuwa kukamatwa kwa askofu huyo ni mapenzi ya papa kwamba kesi kama hiyo inayozua hisia isikilizwe kwa haraka bila kuchelewa.

Papa Francis ameahidi kufanya msako dhidi ya makasisi na wafanyakazi wa Vatican, ambao huwadhulumu watoto wadogo akifananisha vitendo vyao kama vya kishetani.

Mwaka jana aliweka sheria kali dhidi ya watuhumiwa wa udhalilishaji wa watoto katika Vatican.

Msemaji wa Vatican, alisema kuwa uamuzi wa kumpa kifungo cha nyumbani askofu huyo, badala ya kumzuilia katika kituo cha polisi, ulifikiwa kutokana na afya yake.

Kesi ya Wesolowski inatarajiwa kusikilizwa baadaye mwaka huu.