ICC kuanzisha uchunguzi CAR

Haki miliki ya picha
Image caption Mahakama ya ICC inasema ina taarifa za kuaminika kuhusu uhali wa kivita uliotendwa nchini humo.

Mahakama ya kimataifa ya ICC imeanzisha rasmi uchunguzi kuhusu madai ya uhalifu wa kivita katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati.

Mwendesha mkuu wa mashitaka katika mahakama hiyo, Fatou Bensouda, amesema kuwa kumekuwa na ongezeko la matukio ya ubakaji, mauaji na watu kufurushwa kutoka makwao kwa lazima , mateso na maasi mengine tangu mwaka 2012.

Amesema pande zote zimehusika kwenye mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini humo ambao umegeuka na kuwa mzozo wa kidini kati ya waisilamu na wakristo hasa waasi wa Kiisilamu na wakristo.

Takriban robo ya idadi yote ya watu nchini humo wametoroka makwao.

'Watoto jeshini'

Mgogoro ualianza baada ya waasi wa Seleka kuchukua mamlaka kati a nchi hiyo yenye idadi kubwa ya wakristo, machi mwaka 2013.

Kiongozi wa waasi, Michel Djotodia alijiuzulu kama Rais mwezi Januari kufuatia shinikizo kali kutoka kwa viongozi wengine wa kanda hiyo.

Waisilamu, walilazimika kutoroka mashambulizi ya kulipiza dhidi yao yaliyofanywa na wapaiganaji wa kikrsto, waliojulikana kama Anti-balakas.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Catherine Samba Panza alichaguliwa kama Rais wa Muda kumaliza ghasia lakini hali bado haijabadilika

Mwezi jana serikali ya muungano iliundwa , lakini haijamaliza taharuki katika nchi hiyo ambayo imegawanyika kwa misingi ya kidini.

Bi Bensouda, aliyeanzisha uchunguzi wa awali mwezi Februari, alisema ofisi yake imetathmini taarifa za kuaminika kuhusu uhalifu huo.

Bansouda alisema kuwa uhalifu mwingine wa kivita pamoja na uhalifu dhidi ya binadamu, ulijumuisha mashambulizi dhidi ya mashirika ya misaada na kuwatumia watoto kama wanajeshi.

''Orodha ya uhalifu uliotendwa ni ndefu sana. Siwezi, kupuuza madai yanayosemekana kufanywa,'' alisema katika taarifa yake.

"huu unapaswa kuwa ujumbe wa mwisho kwa wanaotenda uhalifu huu kwamba muda wao umekwisha, kilichosalia ni kukabiliwa na sheria,'' aliongeza kusema Bensouda.

Mapema mwezi huu Umoja wa Mataifa ulichukua jukumu la kulinda amani nchini humo kutoka kwa kikosi cha Muungano wa Afrika.