Ugonjwa wa Polio waibuka Pakistan

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waislamu wenye siasa kali wamekuwa wakieneza porojo kuwa chanjo ya polio inatumika kuwahasi Waislamu

Visa 10 vya maradhi ya polio vimethibitishwa nchin Pakistan, na kufanya idadi ya watu waliopatikana na maradhi hayo kwa wakati mmoja katika mwongo uliopita kuwa ya juu zaidi.

Tangu mwaka huu kuanza kumeripotiwa visa 184 vya maradhi hayo ya polio.

Pakistan ni moja ya mataifa matatu duniani yaliyo na visa vingi vya polio .

Maafisa wa Afya wanasema kuwa idadi kubwa ya visa vya Polio vimepatikana katika maeneo ya mashambani Kaskazini Magharibi mwa taifa hilo.

Chanjo za polio zinakabiliwa na changamoto nyingi katika maeneo hayo kwa sababu wapiganaji waislamu wenye itikadi kali wameeneza porojo kuwa chanjo hiyo ni njia mojawapo inayotumiwa kuwahasi Waislamu.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption WHO imependekeza vikwazo kwa raiya wa Pakistan kuhakikisha wamepokea chanjo hiyo

Wafanyakazi kadhaa wa Afya wameuawa nchini humo.

Visa hivyo vipya vimethibitishwa wakati huu ambapo wataalamu wa kimataifa wa maswala ya polio wanakutana mjini London ili kujadiliana hatua za kuchukuliwa dhidi ya Pakistan kwa kukosa kupambana kikamilifu na maradhi hayo.

Miongoni mwa vikwazo vilivyopendekezwa na shirika la Afya Duniani, WHO, raia wote wa Pakistan wanapaswa kutoa vibali vya kuthibitisha kuwa wamechanjwa dhidi ya maradhi hayo kabla ya kusafiri ngambo.