Mgonjwa wa Ebola sio tisho Marekani

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mgonjwa wa kwanza wa Ebola Marekani

Mgonjwa wa kwanza wa ugonjwa hatari wa virusi vya Ebola amegundulika nchini Marekani, imethibitishwa katika mji wa Dallas, Texas.

Maafisa katika kituo cha afya cha Texas katika hospitali ya Presbyterian wamesema mgonjwa ambaye hakutajwa ametengwa katika hospitali hiyo.

Mtu huyo hakuwa mgonjwa aliposafiri kutoka Liberia siku kumi zilizopita kutembelea familia yake inayoishi Marekani.

Alianza kupata dalili za Ebola siku nne baadaye.

Mkurugenzi wa shirika la Marekani linalosimamia na kuzuia kuenea kwa maradhi - CDC - Tom Frieden, aliwahakikishia wale ambao huenda walisafiri na mgonjwa huyo kwenye ndege au kwingineko alikokuwa akisafiri, kuwa mtu huyo alilazwa hospitalini siku nne baada ya kuwasili Marekani.

Image caption Mkuu wa shirika la CDC Tom Frieden amesema mgonjwa huyo sio tisho kwa umma

Alisema kuwa mtu huyo kwa wakati huo akisafiri hakuwa na uwezo wa kumwambukiza ye yote.

Lakini baada ya mtu huyo kuwa mgonjwa ilichukua siku nne kabla ya kulazwa hospitalini na maafisa wa afya sasa wanawatafuta watu wote ambao huenda walikaribiana naye ambao wako katika hatari ya kuwa waliambukizwa maradhi hayo.

Ingawa wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada walioambukizwa maradhi ya Ebola Afrika Magharibi wamerejea Marekani kwa matibabu lakini huyu mgonjwa ni wa kwanza kuwa mgonjwa na maradhi hayo akiwa nchini Marekani.

Shirika la CDC linafanya kila juhudi kuwahakikishia raia wa Marekani kuwa vyombo vya afya nchini Marekani vina uwezo wa kuhakikisha kuwa maradhi hayo hayasambai ko kote.