Tangazo la biashara lazua zogo China

Image caption Polisi wanachunguza ikiwa kampuni hiyo ilivunja sheria ya matangazo ya biashara

Kampuni moja nchini China inakabiliwa na tisho la kutozwa kiwango kikubwa cha faini kwa kuwakodi wanawake kuvua nguo zao kwenye treni mjini Shanghai kwa lengo la kutangaza biashara ya kampuni hiyo kwa abiria.

Katika moja ya video iliyowekwa kwenye mtandao wiki jana, wasichana wawili ghafla walianza kuvua nguo zao na kusalia na nguo za ndani pekee katika treni hiyo iliyokuwa imejaa watu.

Abiria walionekana wakirekodi wasichana hao kwa simu zao za viganjani lakini mwanamke mmoja wa makamo aliwakaripia sana.

Mwanamume mmoja kutoka katika kampuni ya huduma za dobi ambayo wasiahana hao walikuwa wakiitangaza, naye alionekana akiokota nguo za wasichana hao walizokua wanavua.

Baada ya filamu ya wasichana hao wakivua nguo kuenea mitandaoni, polisi waliwasiliana na kampuni hiyo kujibu walichokuwa wanakifanya.

Kampuni hiyo inayotoa huduma za dobi ,kwa jina 'Tidy Laundry', ilipoona ikipata sifa mbaya, iliamua kuomba radhi kwa kosa hilo ikisema kuwa ilinuia tu kutangaza huduma zake kwa wabiria waliokuwa ndani ya treni hiyo.

Taarifa hii ni kwa mujibu wa jarida la Shanghai Daily.

Wamiliki wa kampuni hiyo, wanasema kila aliyehusika kwenye tukio hilo alikuwa muigizaji aliyekuwa amekodiwa.

Hata hivyo huu bila shaka sio mwisho wa masaibu ya kampuni hiyo-polisi wanasema wanachunguza ikiwa ilivunja sheria zinazopiga marufuku matangazo ya kibiasga ambayo yanakera jamii.