Mgonjwa mwingine wa Ebola Ujerumani

Image caption Mgonjwa huyu ni wapili kupatikana na Ebola Ujerumani

Hospitali moja mjini Fanakfurt Ujerumani inamtibu mgonjwa wa Ebola aliyefikishwa nchini humo nyakati za usiku chini ya ulinzi mkali.

Baada ya kuwasili kwa ndege kutoka Afrika Magharibi, mwanamume huyo alifikishwa katika hospitali ya Frankfurt University ambako aliwekwa karantini.

Mwanamume huyo ni daktari kutoka Uganda ambaye aliwatibu wagonjwa wa Ebola nchini Sierra Leone.

Hiki ni kisa cha pili cha mgonjwa wa Ebola kupatikana Ujerumani. Kisa cha kwanza kilikuwa cha mwanamume aliyewasili mjini Hamburg akiwa na Ebola kutoka Afrika Magharibi mwezi Agosti.

Katika kanda ya Afrika Magharibi, zaidi ya watu 3,338 wamefariki kutokana na Ebola ukiwa mlipuko mbaya zaidi wa Ebola kuwahi kushuhudiwa duniani.

Watu 7,178, walithibitishwa kuwa na Ebola nchini Sierra Leone, Liberia na Guinea ikiathirika zaidi kuliko nchi nyinginezo.

Madaktari katika hospitali hiyo wamesema kuwa mgonjwa huyo ameshughulikiwa vyema.