Wanafunzi Hong K. kukutana na serikali

Haki miliki ya picha AFP

Viongozi wa wanafunzi huko Hong Kong wamekubali kukutana na upande wa serikali kujadili malalamiko yao siku tano baada ya maandamano makubwa ya kupigania demokrasia.

Hiyo inafuatia mwaliko kutoka kwa mkuu wa utawala wa Hong Kong CY Leung. Alitoa taarifa hiyo muda mfupi kabla ya kumalizika kwa muda wa mwisho uliowekwa na wanafunzi hao waliotishia kuvamia majengo ya serikali iwapo mkuu huyo hatajiuzulu.

Muda wa mwisho uliowekwa na wanafunzi hao umemalizika salama.

Bwana Leung amesema atabakia madarakani na kuwaonya waandamanaji kuwa watapata matatizo iwapo watavamia majengo ya serikali.

Kumekuwa na makabiliano makali katika eneo la majengo ya serikali ambapo waandamanaji wamekuwa wakiendelea kudai uchaguzi wa haki mwaka 2017.