Jeshi la Somalia na AU wadhibiti Barawe

Image caption Wanajeshi wa Somalia

Wanajeshi wa Somalia wakisaidiwa na vikosi vya Muungano wa Afrika kwa sasa wamechukua udhibiti wa mji wa Barawe ambayo ni ngome ya mwisho ya wanamgambo wa al-Shabab.

Wanajeshi hao waliingia mji wa Barawe ulio kusini magharibi mwa mji mkuu Mogadishu siku ya Jumatatu baada ya kuuzingira tangu siku ya Jumapili.

Sauti za risasi zilisikika mapema Jumatau wakati wanajeshi walikuwa wakiingia mji huo. Ripoti zinasema kuwa kwa sasa mji huo umetulia na magari ya kijeshi kwa sasa yanapiga doria.

Mji wa Barawe haujakuwa chini ya serikali kwa miaka 23 na umekuwa chini ya udhibiti wa al Shabab kwa miaka sita iliyopita.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wanamgambo wa al-Shabab

Gavana na maafisa wa kijeshi waliwahutubia wenyeji leo ambapo walitoa wito wa kuwepo kwa utulivu wakisema kuwa nyakati za al-Shabab zimekwisha.

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia Nicholas Kay alipongeza jeshi hilo la pamoja na kusema kuwa sasa Somalia ina mazuri siku za usoni.

Kutwaliwa kwa mji huo ni pigo kwa kundi la al-Shabab lililo na uhusiano na mtandao wa al-Qaeda.

Al Shabab wamekuwa wakiutumia mji huo kupitisha silaha na chakula na pia kama kituo cha biashara ya makaa.

Muungano wa Afrika pia unasema kuwa al-Shabab waliutumia mji wa Barawe kupanga mashambulizi yao dhidi ya mji mkuu Mogadishu.