Uhaba wa walimu katika mataifa maskini

Image caption Idadi ya wanafunzi inakisiwa kuongezeka katika mataifa yanayostawi katika miaka inayokuja

Ripoti ya Umoja wa mataifa imeonya kwamba uhaba wa walimu katika nchi zinazostawi utazidi kuongezeka kutokana na ongezeko linalotarajiwa la watoto wa kwenda shule.

Shirika la umoja wa mataifa kuhusu elimu sayansi na utamaduni - UNESCO linasema walimu wengine milioni nne waliopokea mafunzo watahitajika iwapo lengo la milenia la Umoja huo la kutoa elimu msingi kwa watoto wote linatarajiwa kufikiwa. Ifuatayo ni taarifa yake Naomi Grimley.

Jumuiya ya kimataifa huenda iisifikie ahadi yake ya kutoa elimu ya msingi kwa kila mtoto ifikapo mwaka ujao.

Hiyo ni kutokana na kwamba watoto milioni 58 bado hawaendi shulenikote duniani. Na kwa mujibu wa ripoti hiyo mpya ya UNESCO, hali hiyo huenda ikazidi kuwa mbaya kutokana na kutarajiwa kuongezeka idadi ya watoto wenye umri wa kwenda shuleni katika miaka ijayo.

Hata kwa nchi yenye uchumi wa kukuwa kama Nigeria, kwa mfano, inahitajika kutafutwa dola bilioni 1.8 nyengine kuwasomesha watoto kufikia 2020.

Ripoti hiyo pia inaonya kwamba tayari nchi nyingi zinawasajili walimu ambao hawakufuzu kwenye taaluma hiyo katika kujarbu kuziba pengo katika mfumo wa elimu.

Nchini Angola, Sudan kusini na Senegal kiwango kisichofika nusu cha walimu hawana mafunzo sahihi, hali inayosababisha lengo hilo la milenia kuwa ahadi ya mbali.