UN:M23 walibaka mamia ya wanawake

Image caption Waasi wa M23 waliweka chini silaha baada ya kushindwa vita

Kikosi cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, kimetuhumu kundi la waasi wa zamani M23 kwa kufanya uovu mkubwa ikiwemo kuwabaka mamia ya wanawake.

Waasi hao pia wanadaiwa kufanya uhalifu dhidi ya binadamu.

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa, inasema kuwa miezi 18 kabla ya kundi hilo la waasi kujisalimisha liliwaua zaidi ya watu 110 na kuwabaka wanawake zaidi ya 160 pamoja na wasichana wadogo.

Inaarifiwa wengi wa wanawake waliobakwa walikuwa wake wa wanajeshi au maafisa wa jeshi.

Waasi wa M23 waliwalenga zaidi maafisa wa eneo hilo waliokataa kushirikiana nao pamoja na vijana waliokata kujiingiza katika harakati za kundi hilo.

Umoja wa Mataifa unatoa wito kwa serikali kuwachukulia hatua wote waliotenda uhalifu huo.