Ebola:Wanajeshi 1,300 karantini Liberia

Image caption Liberia ni moja ya nchi zilizoathirika zaidi na Ebola Afrika Magharibi

Jeshi nchini Nigeria limesema zaidi ya wanajeshi wake elfu moja miatatu wanaofanya kazi chini ya kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Liberia wamewekwa Karantini, baada ya mwanamume mmoja kuingia katika kambi yao na kufariki.

Wabunge wa Liberia wanatarajiwa kujadili ombi la Rais Ellen Johnson-Sirleaf la kutaka kuzuia watu kutembea baada ya nyakati fulani za siku ili ugonjwa huo uweze kudhibitiwa.

Wapinzani wa serikali wamepinga pendekezo hilo wakisema ni la kukandamiza.

Nchini Mali,jaribio la kwanza la chanjo mpya ya Ebola limefanyika.

Na nchini Uhispania, watu wengine saba wamewekwa chini ya uangalizi wa madaktari baada ya kukutana na muuguzi aliyeambukizwa Ebola. Muuguzi huyo inaarifiwa yuko katika hali mahututi.

Mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika kanda ya Afrika Magharibi ni janga la kipekee ambalo halijashuhudiwa hivi karibuni na tangu kugunduliwa kwa janga lengine la ugonjwa wa Ukimwi.

Hii ni kwa mujibu wa afisaa mmoja mkuu wa matibabu nchini Marekani Thomas Frieden.

''Hatua za haraka dhidi ya janga hilo zitahakikisha kuwa ebola haigeuki na kuwa kama janga la HIV,'' alisema mkurugenzi wa kitengo cha udhibiti wa magonjwa nchini Marekani, CDC.

Marais wa Liberia , Siera Leone na Guinea waliomba msaada zaidi wa kukabiliana na ugonjwa huo.

Ugonjwa huo umesabisha vifo vya watu 3,860 wengi wao katika kanda ya Afrika Magharibi.

Zaidi ya wahudumu 200 wa afya ni miongoni mwa watu waliofariki.