Wapenzi wa jinsia moja Kenya wataka usajili

Jamii ya wapenzi wa jinsia moja pamoja na watu waliobadili jinsia yao nchini Kenyan inataka serikali kulazimishwa kulipatia usajili shirika walilozindua kutetea masilahi yao.

Wanasema ikiwa serikali itakosa kufanya hivyo itakuwa ni ukiukwaji wa haki zao.

Katika kesi yao waliyofikisha mahakamani, kundi hilo linasema haki zao zimelindwa na katiba ambayo inajali utu , usawa na haki pomoja na kuwaruhusu watu kushirikiana.

Kundi hilo linasema kuwa ni ukiukwaji wa katiba ya Kenya kwa serikali kukataa kusajili shirika hilo la wapenzi wa jinsia moja.

Kulingana na stakabadhi zilizowasilishwa mahakamani, shirika hilo, linasema kwa watu wa jinsia moja na wale wanaotaka kubadili jinsia yao wanapaswa kusajiliwa ili waweze kutetea maslahi yao.

Hata hivyo serikali inasisitiza kuwa shirika hilo linapaswa kutimiza matakwa ya usajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yanasema kuwa kila anayetaka kusajiliwa lazima apate idhini ya mkurugenzi wa sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali.