Msomi mkenya Profesa Mazrui afariki

Image caption Profesa Mazuri alisifika sana kwa kuangazia tamaduni za kifarika kwa dunia nzima

Msomi mashuhuri wa Kenya,Profesa Ali Mazrui ameaga dunia nchini Marekani.

Mazrui alikuwa msomi wa maswala ya kisiasa, utamaduni wa kiafrika na maswala ya dini ya kiisilamu.

Mazrui aliyekuwa na umri wa miaka 81 alifariki nchini Marekani ambako amekuwa akiishi baada ya kuugua kwa mda mrefu.

Duru zinasema kuwa Profesa Mazrui atazikwa mjini Mombasa Pwani ya Kenya alikozaliwa.

Kabla ya kifo chake Marehemu Mazrui alikuwa mhadhiri katika chuo kikuu cha Binghamton mjini New York.

Kwa miaka mingi Mazrui alisikizwa na viongozi wa mataifa mengi ya afrika na ya kigeni, akizungumzia nafasi ya Afrika katika dunia nzima.

Alichapisha vitabu vingi na pia kuandika nyaraka mbali mbali kuhusu siasa za Afrika, athari za siasa kwa dini ya kiisilamu na uhusiano kati ya mataifa ya Kaskazini na Kusini.

Alipigia debe wazo la Afrika kuwa huru na alikosoa mataifa yanayonyakua rasilimali za Afrika na kunyanyasa watu wake.

Mapema mwaka wa1980, aliandika na kutangaza makala kwa BBC yenye mada, 'The Africans - a Triple Heritage' ambapo alionyesha Afrika kuwa bara lenye mchanganyiko wa imani ya kiisilamu, mfumo wa maisha ya kimagharibi na utamaduni asilia.