Grace Mugabe:'Matebele wapenda ngono'

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Dr Grace Mugabe na Mumewe Rais Robert

Mke wa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe Grace Mugabe siku hizi ni dokta, cheo kilichozua mtafaruku nchini mwake akikinzwa katika udaktari wake wa masuala ya sosholojia alioupatia katika chuo kikuu cha nchi hiyo, amewatemea cheche wanaume wa eneo la Matabeleland nchini humo kuwa ni hodari wa kuoa wake wengi kila uchao na kuwazalisha watoto na kushindwa kuendeleza makazi yao .

Dokta Mugabe aliyasema hayo katika mkutano wa hadhara unaokisiwa kuhudhuriwa na watu wapatao elfu nne katika viwanja vya Gwanda mapema wiki hii. Dokta Mugabe amewashangaa wanaume hao kutoka kabila la Ndebele kwa kuwa maarufu wa kuzalisha na kuwatelekeza watoto bila matunzo yoyote huku wakiendekeza ngono Zaidi.

Dr Grace anasema ni jambo la kawaida kumkuta mwanamume ana wake watano hadi kumi na kuuita ni upuuzi mkubwa.

Pmaoja na hayo ,Dr Mugabe amewashutumu pia wanaume hao wa Matabele kusini kwa kushindwa kufanya maendeleo yao binafsi na badala yake mawazo yao ni kusafiri kuelekea Africa Kusini hasa katika jiji la Johannesburg kufanya kazi za nyumbani.

Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miaka miwili familia ya Mugabe kuwakosoa wanaume wa Matebele hadharani kwa kukimbilia Africa Kusini kuajiriwa kama watumishi wa ndani.

Mara ya kwanza alikua ni Rais Mugabe aliyezua mjadala mkali kutoka kwa watu wa Matebele, ambapo alitoa kauli kama za mkewe katika eneo hilo hilo mwaka wa jana.Dr Grace Mugabe pia amewashutumu wanaume wa eneo hilo kwa ubakaji na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake.

Pamoja na kuwatemea cheche hizo Dokta Grace Mugabe alishangazwa na umati mkubwa uliojitokeza kumlaki katika mkutano huo , huku wakimpigia makofi mazito,akiwemo waziri wa michezo na utamaduni Andrew Langa,mwenyekiti wa ZANU PF Simon Khaya Moyo na waziri Abdenico Ncube.