Mwizi wa mapenzi akamatwa Austria

Image caption Tijan Sonko

Polisi nchini Austria wanawahoji wanawake ambao wamehadaiwa na mwanamume mwenye mazoea ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanawake wengi tu.

Mwanamume huyo raia wa Gambia mwenye umri wa miaka 28 ameoa wanawake watatu huku akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na wanawake wengine 15

Kwa mujibu wa mtandao wa 'ASN American street news', Tijan Sonko, alikamatwa tarehe mbili mwezi Oktoba katika uwanja wa ndege mjini Vienna akiwa anarejea kutoka nchini Gambia.

Pia anatuhumiwa kwa udanganyifu baada ya kuwapora wapenzi wake yuro 38,000.

Kadhalika ameshtakiwa na kosa la wizi na kutumia vitambulisho bandia.

Kulingana na shirika la habari la Austria alitumia bima ya afya ya rafiki yake kudai faida anazopata mtu ambaye hana ajira kutoka kwa serikali.

Mwanamke mwenye umri mdogo sana kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Sonko ana umri wa miaka 22 huku mzee zaidi akiwa na umri wa miaka 44.

Msemaji wa polisi mjini Vienna alisema kuwa wanawake wote waliohusika na Sonko wanahojiwa kubaini ikiwa walidanganywa na kuibiwa.

Sonko alidai kuwa alihitaji pesa ili kuwatumia jamaa wake nchini Gambia na wapenzi wake kadhaa walimpa pesa na vifaa vingine vya thamani.

Ameishi mjini Vienna tangu Septemba mwaka 2010.

Udanganyifu wake ulijulikana wakati wanawake wawili walijuana kupitia Facebook, na kugundua kuwa walikuwa wanatoka na mwanamume mmoja.

Sonko ana watoto wanne mjini Vienna, na wapenzi wake wawili wanaaminika kuwa na mimba .

Ana mke nchini Gambia, na anaaminika kumpa zawadi na mapambo mengine aliyopewa na wapenzi wake wa Austria.

Tangu picha yake kuchapishwa na polisi, wanawake wengine wawili wamejitokeza wakisema na wao wamehadaiwa.