Maji ya kuosha wafu,kivutio cha biashara

Image caption mortuary

Katika tukio la kushangaza na la kutaka kujiongezea mapato pamoja na kushamiri kwa biashara,wafanyibiashara wawili katika mtaa wa Lobengula nchini Zimbabwe walizozania maji machafu yanayopatikana baada ya kuosha wafu ambayo huyatumia kuvutia wateja.

Wawili hao waliojulikana kama ViolaTshuma na Molene Hadebe walikabiliana vilivyo baada ya Hadebe kuchukua kiwango kikubwa cha maji hayo ya kuosha maiti kabla ya mwenzake kuwasili.

Wafanyibiashara hao wanaodaiwa kuwa rafiki wakubwa walipata maji hayo kutoka chumba kimoja cha mazishi katika mji wa Bulawayo kwa biashara yao ya kila siku.

Kulingana na wafanyibiashara wengine maji hayo huuzwa kwa wafanyibishara na wanawake wanaotumia kufanya tambiko.

Maji hayo pia hutumika kuwazima wanaume walio wakali kwa wake zao baada ya kubaini kwamba wake hao wanawanyemelea wanaume wengine.

Wafanyibiashara waliohijiwa pia walibaini kuwa maji hayo pia hutumiwa kuosha matunda na hata nyanya ili kuwavutia wateja wengi kama wale wanaouhudhuria mazishi.