Ebola yahatarisha kizazi cha vijana

Rais Sirleaf wa Liberia

Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, ameziomba nchi zote kusaidia kupambana na virusi vya Ebola.

Kwenye barua aliyoandikia kipindi kimoja cha BBC, anasema ni kwa masilahi ya dunia nzima kujiunga na jitihada hiyo, kwa vile ugonjwa huo hautambui mipaka:

"Ni wajibu wetu sote kama raia wa ulimwengu, kwamba hatutowaacha ma-milioni ya watu wa Afrika Magharibi kujihami wenyewe dhidi ya adui ambaye hawamjui na hawawezi kujikinga naye.

Wakati wa kuzungumza tu na kujadili, umepita.

Kitachonusuru nchi yangu na jirani zetu na janga jengine, ni kuchukua hatua kwa jitihada kubwa."

Rais Sirleaf anasema Ebola imesimamisha shughuli za taifa lake na kuuwa maelfu ya watu katika miezi sita tu.

Piya alionya kuwa kizazi chote cha vijana wa Afrika kiko hatarini kwa sababu ya maafa ya kiuchumi, wakati watu hawawezi kuvuna na masoko na mipaka imefungwa.