West Brom na Man U kibaruani leo

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Liverpool vs QPR

Baada ya Liverpool kupata ushindi wa bahati nasibu kutoka kwa Queens Park Rangers na malalamiko ya Boss wa Swansea Garry Monk dhidi ya analoliita tendo la kujiangusha la winga wa Stoke City, Victor Moses, leo tunashuhudia mtanange mwingine mkali kati ya West Brom na Manchester United itakayomkosa Wayne Rooney anayetumikia adhabu ya Kadi nyekundu.

Yako mambo ya kukumbukwa zinapokutana timu hizi mbili, West Brom iliwahi kuwachapa United mara moja tu katika Premier League.

Leo ni jumatatu ni vema kukumbuka kuwa West Brom imeshinda mechi mbili tu kati ya 18 ilizocheza katika siku ya jumatatu na wakipata bao moja watatimiza magoli 500 katika Premier League.

West Brom wakiwa kwao wamepoteza mchezo mmoja tu katika mitano ambapo walishinda michezo miwili na kutoka sare michezo miwili.

Upande wa Manchester United wakishinda mechi ya leo utakuwa ni ushindi wao wa tatu mfululizo katika mwaka huu.

Lakini wakiupoteza mchezo wa leo itakuwa ni mechi ya tano kuipoteza katika mchezo wao wa nje ambayo ni matokeo mabaya ndani ya miaka mitano. Ni miaka 18 iliyopita tangu Manchester United ilipopoteza michezo sita bila ushindi katika Premier League.