Aliyekuwa amepooza atembea tena

Image caption Darek Fidyka

Mwanamume aliyekuwa amepooza sasa ameweza kutembea tena baada ya kupokea matibabu yaliyohusisha kutoa seli kutoka kwa pua lake na kuzipandikiza kwenye uti wake wa mgongo.

Darek Fidyka, alipooza kutoka kwa kifua chake hadi miguuni baada ya kudungwa kisu katika shambulizi mwaka 2010. Sasa anaweza kutembea ila kwa usaidizi mdogo.

Matibabu hayo ya kwanza ya aina yake yalifanywa na madaktari wapasuaji nchini Poland wakisaidiana na wanasayansi kutoka mjini London, Uingereza.

Taarifa za matibabu hayo zimechapishwa katika jarida la matibabu ya upandikizaji wa seli.

Darek Fidyka, 40, alipooza baada ya kudungwa kisu mara mingi kwenye mgongo wake mwaka 2010.

Alisema kwake yeye kuweza kutembea tena ni jambo la kumtia moyo sana, akiongeza kuwa '' Wakati mtu anashindwa kuwa na hisia katika nusu ya sehemu yake ya mwili, unakuwa ni kama hujiwezi. Lakini wakati hisia zinapoanza kurejea unahisi ni kama umezaliwa upya.''

Profesa Geoff Raisman, mwenyekiti wa kitengo cha nurolojia chuo kikuu cha College London, ndiye aliyeongoza upasuaji huo.

Alisema matokeo ya utafiti huu ni ya kufurahisha sana hata kuliko binadamu kutembea mwezini.

Wanasayansi hao walitumia seli zilizo ndani ya pua ambazo zinamsaidia mtu kuweza kunusa kwa kuzipandikiza kwenye uti wa mgongo wa Darek.

Seli hizo zilisaidia seli mpya za neva kukuwa na sasa zitaendelea kuzaana na kuufanya uti wa mgongo kuwa imara ikiwa ndiyo sehemu tu ya mwili iliyo na uwezo wa kufanya hivyo.

Matiabu hayo yalifanywa na madakatari nchini Poland kwa ushirikiano na wanasayansi kutoka nchini Uingereza.