Ebola:Marekani kuwapima abiria wa nje

Haki miliki ya picha PA
Image caption Wasafiri wakiwasili katika moja ya viwanja vya ndege

Sheria mpya za Marekani zinazowataka abiria watakaopitia moja ya viwanja vya ndege kutoka nchi tatu za Afrika Magharibi zilizoathirika zaidi na ugonjwa wa Ebola, zimeanza kutumika.

Wasafiri kutoka Sierra Leone, Liberia au Guinea kwa sasa lazima watue uwanja wa ndege wa O'Hare, Chicago, JFK, Newark, Dulles wa Washington au Atlanta, ambako watafanyiwa uchunguzi wa kina wa afya zao.

Shirika la Afya Duniani linatarajiwa kufanya mkutano wa dharura baadaye.

Mlipuko wa sasa wa virusi vya ebola tayari umeua watu zaidi ya 4,500.

Vifo vingi vimetokea katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone.

Wasafiri kutoka nchi hizo watapimwa joto la miili yao kama sehemu ya mpango wa kuwachunguza afya zao, licha ya wataalam kuonya kuwa hatua kama hizo zinaweza zisitoe matokeo yanayotarajiwa.

Hatua mpya za kiusalama zimekuja wakati wasiwasi unaongezeka miongoni mwa umma nchini Marekani, ambako watu watatu waliambukizwa virusi vya Ebola na mtu mmoja amekufa kutokana na virusi hivyo.