Wenye vichwa vikubwa wanyanyapaliwa

Image caption Mama akiwa amempakata mtoto wake mwenye ulemavu wa kichwa kikubwa hospitalini nchini Tanzania.

Wanawake nchini Tanzania hasa wale ambao bado wapo kwenye umri wa kuzaa wameshauriwa kula vyakula vyenye folic acid zikiwemo mboga za majani na matunda ili kuwaepusha na matatizo ya kuzaa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi. Wito huu umetolewa wakati ambapo nchi zaidi ya 46 zinaadhimisha siku ya mtoto mwenye matatizo hayo.

Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya afya, tatizo la kujifungua mtoto mwenye kichwa kikubwa na mgongo wazi linaepukika. Kinachotakiwa kwa kina mama wajawazito ni kupewa uelewa wa kutosha kuhusu lishe hasa katika kipindi cha ujauzito.

Hata hivyo, inaonekana kunahitajika kazi ya ziada kwa sababu uelewa miongoni mwa kina mama bado ni mdogo. "Sisi tunahisi kwamba uelewa ni mdogo sana, na tunatakiwa sasa hivi kueneza hii elimu kwamba ni lazima mama ambaye anatarajiwa kushika ujauzito au msichana mdogo ambaye anatarajia kuolewa na kuja kuzaa basi aanze kutumia hizi folic acid tangu wakati huo na asingojee mpaka apate ujauzito. Mtoto wakati ule anaumbika siku za mwanzo mwanzo anaweza kupatwa na hali hii," amesema Abdulhakim Bayakubu ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Wazazi wenye watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.

Ingawa watoto wanaozaliwa na matatizo haya wanatoka sehemu mbalimbali nchini Tanzania, lakini takwimu zinaonyesha kuwa wagonjwa wengi wanatokea katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Mwanza. Mbali na tatizo la lishe, Dr. Marks Mwandosi ambae ni mtaalamu wa upasuaji katika hospitali ya Muhimbili anasema mtoto pia anaweza kuzaliwa katika ule mfumo wake wa maji ya kwenye ubongo ambayo yanalinda ubongo, yakawa hayazunguki katika mfumo wa kawaida. Hii inatokana na mtoto jinsi alivyoumbwa tumboni. Inawezekana ikawa kuna kuzibwa au yakawa hayanyonywi vizuri au yanatengenezwa mengi.

Baadhi ya kina mama ambao ndio walezi wa watoto wenye matatizo ya kichwa kikubwa na mgongo wazi wamemwambia mwandishi wa BBC Aboubakar Famau kwamba wanakabiliwa na tatizo la unyanyapaa katika jamii huku miongoni mwao wakikiri hata kuvunjika kwa ndoa zao baada ya kujifungua watoto wenye matatizo hayo.

Mwajuma Hassan Makame amelazimika kulea mtoto mchanga katika wodi ya hospitali ya Muhimbili huku akimuuguza binti yake wa miaka kumi. Katika mazingira ya kawaida, hairuhusiwi mtoto mdogo kuingia hospitalini hasa anapokuwa hana tatizo la kiafya kwa kuhofia kuhatarisha maisha yake.

"Sina wa kunisaidia huyu mtoto. Ninao jamaa zangu lakini huruma ni ndogo. Nina dada zangu baba mmoja mama mmoja hapa Dar es Salaam, lakini hawaji hata kuniangalia. Yaani nisipokuwa na chakula cha hospitali, basi nimelala. Siletewi chakula na ndugu. Huu ni mzigo wangu pekee yangu. Babake yuko, lakini amenisusia muda mrefu, nahangaika pekee yangu," amefafanua Mwajuma huku machozi yakimlengalenga.

Tatizo la watoto wanaozaliwa na ugonjwa huu linaonekana kuwa kubwa nchini Tanzania. Kila watoto elfu nne wanaozaliwa kwa mwaka, wawili au watatu miongoni mwao wana tatizo hilo. Takwimu zinaonyesha kwamba hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Muhimbili iliyopo jijini Dar es Salaam nchini Tanzania inapokea watoto takriban 5 mpaka 6 kwa wiki. Hata hivyo, licha ya tatizo hilo kuwepo katika jamii, imedhihirika kwamba nchini Tanzania, kuna vituo vinne tu vya matibabu hayo.

Hali hii ndiyo iliyofanya maadhimisho ya siku ya mtoto mwenye kichwa kikubwa na mgongo wazi ya mwaka huu ambayo yanatarajiwa kufanyika hapo kesho kupewa kauli mbiu ya 'matibabu kwa wote,' ikiwa na lengo la kuitaka serikali angalau kuongeza vituo vya matibabu nchini kwa wagonjwa hao.