Wauguzi wa Ebola hawafai kunyanyaswa

Ebola New York Haki miliki ya picha Getty

Afisa mwandamizi wa afya wa Marekani amelalamika juu ya hatua za baadhi ya majimbo ya Marekani, za kuwaweka karantini watu wote wanaorudi kutoka nchi ya Afrika Magharibi iliyoathirika na Ebola - ambao walikaribiana na wagonjwa wa Ebola.

Dakta Anthony Fauci - mkurugenzi wa taasisi ya taifa inayohusika na magonjwa yanayoambukiza - alisema hatua hiyo inaweza kuzuwia wafanyakazi wa utabibu kwenda Afrika Magharibi kusaidia kupambana na janga hilo.

Alisema njia bora ya kuwakinga Wamarekani ni kuidhibiti Ebola Afrika.

Muuguzi wa Marekani, ambaye aliwekwa karantini baada ya kurudi kutoka Sierra Leone, alisema Jumamosi kuwa aliyotendewa kwao yamemfanya ajihisi kama mhalifu.

Alikaguliwa na kukutikana hana Ebola hadi sasa.

Alitengwa uwanja wa ndege kwa saa 7 na kupewa biskuti moja kula.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Samantha Power, ambaye sasa yuko safarini Afrika Magharibi, alisema wafanyakazi wa utabibu hawafai kunyanyaswa kwa kazi waliyofanya.