Wanaharakati wa demokrasi wafungwa Misri

Mwanaharakati wa demokrasi akitokeza mahakamani nchini Misri Haki miliki ya picha AP

Mahakama ya Misri yamewapa hukumu ya kifungo cha miaka mitatu wanaharakati 23 wanaotetea demokrasi - kwa kufanya maandamano bila ya kibali.

Mashtaka waliyokabili ni pamoja na kuhatarisha usalama wa raia na kuharibu mali ya watu.

Kati yao ni wanaharakati wawili maarufu - Yara Sallam na Sanaa Seif.

Mwaka jana serikali ya Misri ilianzisha sheria iliyopiga marufuku maandamano yanayofanywa bila ya kibali cha polisi.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za kibinaadamu, Amnesty International, limesema kesi hiyo ni kiini macho tu na ni mfano kuonesha kuwa wakuu hawataki kuona upinzani wa aina yoyote.