Ban ataka watu waache unyanyapaa

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon amezitaka nchi duniani kuacha tabia ya unyanyapaa kwa madaktari na manesi waliofanya kazi katika nchi zilizoathiriwa na ugonjwa wa Ebola na kuwalazimisha kwenda karantini pindi warejeapo nyumbani.

Akizungumza katika mji mkuu wa Ethiopia Adiss Ababa,Ban amewaelezea wafanyakazi wa namna hiyo kuwa ni wa kipekee mno,marafiki wazuri na si vyema kuwatenga.

kauli hiyo inakuja baada ya mratibu wa ugonjwa wa Ebola Africa Magharibi Anthony Banbury,kuzitaka serikali kutofanya lolote ili kuepusha maelfu ya wafanyakazi wa afya ambao wanatarajiwa kujiunga wasikate tamaa kabla hawajaanza kazi yenyewe.

Mwishoni mwa juma lililopita nesi raia wa Marekani aliwekwa karantini baada ya kuwa alifanya kazi nchini Sierra Leone na kudai kuwa alikuwa akitendewa kama yeye ni mhalifu na kudai kuwa atakwenda mahakamni kushtaki kwa alichotendewa,ingawa maafisa wenziwe wa afya wanadai huenda akaruhusiwa kurejea uraiani siku za karibuni.