Ukosefu wa dawa kuathiri afya Tanzania

Image caption Hospitali ta Taifa Muhimbili, Dar es Salaam, Tanzania

Bohari ya Dawa nchini Tanzania, MSD imeripotiwa kuwa imesitisha utoaji wa dawa muhimu kwa taasisi za afya za serikali hadi hapo deni la shilingi bilioni 90 linalodaiwa na wakala huyo litakapolipwa na taasisi hizo.

Sikika ambalo ni shirika lisilo la kiserikali linalohimiza huduma bora za afya nchini Tanzania limeeleza Jumapili kwamba kiasi kikubwa cha fedha kinachodaiwa na MSD kime mamlaka hiyo ya usambazaji dawa kushindwa kununua dawa kwa ajili ya zahanati, vituo vya afya na taasisi nyingine za tiba nchini kote.

Image caption Mama akimnyonyesha mtoto wake hospitalini

Mkurugenzi Mtendaji wa Sikika, Irenei Kiria amesema shirika lake lina taarifa rasmi kwamba MSD inaweza kutoa dawa na vifaa vingine vya tiba pale madeni yanayodaiwa na wakala huyo yatakapolipwa, na kwamba hatua ya MSD ni kuleta msukumo kwa taasisi za tiba kulipa madeni yao, na kuendelea kupata huduma kutoka MSD. " Kile kinachotokea kina madhara makubwa kama hakitashughulikiwa kwa uangalifu.Serikali inatakiwa kutoa fedha kwa wakati kwenda hospitali za umma ili ziweze kuilipa MSD."

Hivi karibuni MSD ilisema miongoni mwa taasisi za tiba zinazodaiwa na wakala huyo ni pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili kiasi cha shilingi bilioni 8 hali ambayo imesababisha MSD kusita kuendelea kununua dawa muhimu kwa ajili ya hopsitali hiyo zikiwemo dawa za kutibu wagonjwa wa figo.