Akata rufaa dhidi ya hukumu ya ushoga

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Anwar Ibrahim

Kiongozi wa upinzani nchini Malaysia, Anwar Ibrahim, amefika mahakamani kukata rufaa dhidi ya hukumu inayomkabili kuwa alishiriki ngono na mtu wa jinsia sawa.

Naibu waziri mkuu wa zamani aliyeshtakiwa kwa kufanya mapenzi na mshirika wake mmoja wa kisiasa alihukumiwa miaka mitano gerezani.

Bwana Anwar anadai kuwa mashtaka hayo yalichochewa na maadui wake wa kisiasa.

Mamia ya wafuasi wake wamesongamana mahakamani kuandamana dhidi ya hukumu iliyotolewa dhidi yake.

Wafuasi wake wanaendelea kuuza tisheti zilizoandikwa kuwa wanaitisha haki ya Bwana Anwar.

Nje ya mahakama utadhani ni mkutano wa hadhara wala sio kesi inayohusiana na uhalifu wa mapenzi.

Ushoga ni haramu katika taifa hili lenye Waislamu wengi lakini ni vigumu sana kupata watu wameshtakiwa.

Mawakili wa Bwana Anwar wanatarajiwa kuwasilisha mahakamani kuwa uchunguzi wa DNA uliotumiwa ulivurugwa katika juhudi za maadui wake wa kisiasa kumharibia sifa.

Maafisa wa Serikali wamekanusha kuhusika katika kesi hiyo na wanasema kuwa kesi ya Bwana Anwar imeshughulikiwa na Mahakama huru.

Mwanasiasa huyo mkongwe ameshtakiwa kuwa alifanya tendo la ngono na mshirika wake wa kisiasa mwanamume.

Hili ni shtaka la pili la ushoga linalomkabili Bwana Anwar tangu atimuliwe Serikalini mwaka 1998.