Ann Cotton atuzwa kwa kusaidia wasichana

Image caption Ann Cotton amekua akiwasaidia wasichana waishio katika jamii hasa za vijijini

Aliyekua mwanzilishi wa Kampeni kuhusu kutoa kipaumbele kwa elimu ya mtoto wa kike barani Afrika amepatiwa tuzo kubwa ya kimataifa.

Ann Cotton, aliyeanzisha kampeni kwa ajili ya elimu kwa mtoto wa kike (camfed), ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya WISE katika mkutano mkubwa unaohusu maswala ya elimu nchini Qatar.

Mradi wa mwanamama huyo umewagusa watoto zaidi ya milioni tatu katika nchi tano za kusini mwa jangwa la Sahara.

Mradi huo umenia kuelimisha wasichana kupambana na umasikini na kuwainua kufahamu maswala ya afya.

Taasisi ya Camfed International iliyoanza mwaka 1993, inawasaidia wasichana hasa waishio vijijini nchini Ghana,Malawi,Tanzania,Zambia na Zimbabwe.

Makao makuu ya taasisi hiyo yako nchini Uingereza husaidia kuwafanya wasichana kuendelea na masomo hivyo hutoa misaada ya karo za shule kwa ajili ya wasichana, kununua vitabu na sare .

Hata hivyo tafiti zinasema bado mamilioni ya wasichana hawana elimu na tatizo hili liko zaidi nchi za kusini mwa jangwa la Sahara.