70% ya Mahabusu Nigeria hawajashtakiwa

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Baadhi ya magereza nchini Nigeria yako katika hali mbaya kiasi cha kuhatarisha usalama

Asilimia 70 ya Mahabusu kwenye Magereza nchini Nigeria bado wanasubiri kufikishwa mahakamani .Msemaji wa magereza amesema kati ya mahabusu 56,785 nchini humo ,Mahabusu 17,775 pekee wamehukumiwa huku wengine wakisubiri kufikishwa mahakamani, Ripoti ya Premium Times imeeleza.

Ofisa uhusiano wa Idara ya magereza ,Ope Fatinikun ametoa kauli hiyo alipozungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa idara ya magereza inakabiliwa na changamoto ya kutokuwepo kwa bajeti ya kutosha .

Fatikun amesema jela zinahitaji kujengwa upya kwa kuwa ziko katika hali mbaya, jela hizo zinatakiwa kumaliziwa hasa zile zilizoanza kujengwa zaidi ya miaka thelathini iliyopita.

Changamoto nyingine iliyoelezwa ni kukosekana kwa silaha kwa ajili ya Operesheni mbalimbali hasa kunapokua na tishio la usalama kwenye magereza.

Fatikun amesema Vifaa vyao vimeshambuliwa na kuchomwa moto , maafisa 16 wa magereza wameuawa tangu kuanza kwa mashambulizi ya Boko Haram.