8 wafariki wakifungwa kizazi India

Haki miliki ya picha ALOK PUTUL
Image caption Upasuaji huo ulifanywa kuwafunga vizazi wanawake zaidi ya 80

Wanawake 8 wamefariki na wengine 50 wanaugua baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuwafunga vizazi nchini India.

Wanawake hao walielezea kuhisi maumivu makali na homa punde baada ya kupewa matibabu hayo ya upasuaji wa kuwafunga uzazi katika kliniki ya kiserikali huko eneo la katikati mwa India Chhattisgarh.

30 miongoni mwa walio hospitali hapo wanasemekana kuwa katika hali mahututi.

Idara ya Afya nchi humo imeamuru uchunguzi ufanyike mara moja.

Zaidi ya wanawake 80 walishiriki katika upasuaji huo wa kuwazuia kupata uja uzito Jumamosi katika hospitali hiyo ya kijijini Pendari huko Chattisgarh.

Baadhi ya wanavijiji wanadai shughuli hizo za upasuaji zilifanywa na daktari mmoja na msaidizi wake katika mda wa masaa 6 tu hivyo wanahoji iwapo ziliendeshwa vyema.

Miili ya Waliofariki ingali inafanyiwa uchunguzi .

Wanaougua wanapewa matibabu katika hospitali tofauti katika eneo hilo.

Waziri wa Afya katika jimbo hilo ameiambia BBC kuwa wanafanya wawezalo kuokoa maisha ya wanaougua na wameunda jopo litakalochunguza kilichosababisha hali hiyo isiyo ya kawaida.

Serikali ya India hufanya utaratibu wa mara kwa mara wa kutoa kwa ujumla huduma kwa wanaohitaji operesheni hizo za kufunga kizazi kama njia moja ya kujaribu kudhibiti ongezeko kubwa la idadi ya watu nchini humo.