Youtube: kutoa huduma bila matangazo

Image caption Youtube itawawezesha watumiaji wake kupata huduma bila kuingiliwa na matangazo ya biashara

Mtandao wa kijamii wa YouTube unaomilikiwa na kampuni ya Google, umeanza kutoa huduma ya kulipia inayowawezesha wateja kusikiliza muziki moja kwa moja mtandaoni bila kuingiliwa na matangazo ya biashara pamoja kupakua nyimbo hizo na kuzisikiliza kwenye kompyuta bila kuwa na internet.

Huduma hiyo ijulikanayo kama Music Key itagharimu pauni 9.99 kwa wateja wa Uingereza kwa mwezi na pia itawapa uanachama wa kuitumia wateja wa huduma nyingine ya Google ijulikanayo kama Google Play All Access, ambayo huwezesha wateja kupakua nyimbo nyingi kadri iwezekanavyo.

Inarajiwa kutoa changamoto kubwa ya kiushindani kwa huduma nyingine za aina hiyo kama Spotify, Rdio, Beats Music na nyinginezo zinazolenga soko la kusikiliza muziki kupitia mitandao.

Kuzinduliwa kwake kumecheleweshwa na mvutano na makampuni yanayofyatua muziki.

Hata hivyo Google imesema imesaini makubaliano na makampuni mengi ya kufyatua muziki kote duniani.