Uchina yatoa msaada zaidi wa Ebola

Wabeba maiti wajitayarisha Monrovia kabla ya kwenda kumzika mama aliyekufa kutokana na Ebola Haki miliki ya picha GETTY IMAGES

Uchina imeongeza msaada wake katika shughuli za kupambana na Ebola Afrika Magharibi kwa kutuma wafanyakazi wa utabibu 160 huko Liberia.

Wafanyakazi wa utabibu ambao wengi wao ni wanajeshi, watawekwa katika kituo cha ukaguzi na matibabu kilichojengwa na Uchina yenyewe katika mji mkuu wa Liberia, Monrovia.

Ubalozi wa Uchina ulieleza kuwa wafanyakazi hao waliowasili hivi karibuni walipata uzoefu wa kutibu homa ya SARS ilipozuka Asia zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Uchina imekuwa ikilaumiwa kuhusu janga la Ebola - kwamba haikutoa msaada wa kutosha na msaada wenyewe unachelewa.