Rais Obama athibitisha kifo cha Kassig

Image caption Rais Barack Obama wa Marekani

Rais Barack Obama amethibitisha kifo cha mfanyakazi wa shirika la kutoa misaada la Marekani Abdul-Rahman Kassig, ambaye ameuawa kwa kukatwa kichwa na kuonyeshwa katika video iliyorushwa na kundi la Islamic State (IS).

Bwana Obama amekitaja kitendo hicho kuwa "uovu uliopitiliza" na kutoa salaam zake za rambirambi kwa familia ya Bwana Kassig, aliyekuwa na umri wa miaka 26, ambaye alitekwa nyara nchini Syria mwaka jana.

Video hiyo ambayo imethibitishwa na Ikulu ya Marekani, inamwonyesha mtu aliyejificha uso akiwa amesimama juu ya kichwa cha Bwana Kassig.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Abdul-Rahman(Peter) Kassig akionyeshwa katika picha akigawa chakula kwa wakimbizi nchini Lebanon Mei 2013

Pia inaonyesha kukatwa vichwa kwa raia 18 wa Syria waliotambuliwa kama maafisa wa jeshi na marubani.

Rais Obama amempongeza Bwana Kassig kama mtu wa kutoa msaada kwa watu wengine na kusema " alichukuliwa kwetu katika kitendo cha uovu wa kupitiliza uliofanywa na kikundi cha kigaidi ambacho ulimwengu unakihusisha na unyama".

"leo tunatoa sala zetu na rambirambi kwa wazazi na familia ya Abdul-Rahman Kassig, ambaye pia tulimjua kwa jina la Peter," amesema.

Kauli ya Bwana Obama imekuja wakati akirejea Marekani kutoka Australia ambako alikuwa akihudhuria kikao cha viongozi wa nchi za G20.

Kikundi cha IS, ambacho kinadhibiti sehemu kubwa ya Syria na Iraq, mpaka sasa kimewaua mateka watano kutoka nchi za magharibi.

Wengine ni Waingereza Alan Henning na David Haines, na waandishi wa habari wa Marekani James Foley na Steven Sotloff.

Mauaji hayo yalitekelezwa na mtu anayeaminika kuwa Mwingereza. Ndevu za mtu huyo zinafanana na wapiganaji walioficha nyuso zao wakiwa wamepigwa picha ya video wakimwonyesha Bwana Kassig.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wanamgambo wa Shia nchini Iraq wakipiga bunduki zao wakati wa mapigano na kundi la Islamic State katika eneo la Jurf al-Sakhar

Tofauti na video zilizotolewa siku za nyuma na kundi la IS, video hii mpya inaonyesha sura za wapiganaji wengi wa jihad na wanaonyesha sehemu yake kuwa ni Dabiq katika jimbo la Aleppo nchini Syria.

Bwana Kassig alikuwa askari wa zamani wa Marekani ambaye alitumikia jeshi la nchi hiyo nchini Iraq.

Baadaye alifundishwa kama mtaalam wa matibabu ya dharura na kuanzisha shirika la kukabiliana na matukio ya dharura na msaada (Sera), likisaidia kusambaza misaada katika makambi yaliyo katika pande zote mbili za mpaka wa Syria.

Alikuwa akiandaa mradi kwa ajili ya shirika lake la Sera alipotekwa mwezi Oktoba 2013 wakati akisafiri kuelekea mashariki mwa Syria.