Njama ya ulanguzi wa masalia ya mtoto yatibuka

Image caption Picha za X-ray zikionyesha masalia yaliyotarajiwa kusafirishwa kwenye maboxi

Polisi nchini Thailand wanasema kuwa wamarekani wawili wametoroka nchini humo baada ya jaribio lao la kutaka kutoweka na masalia ya mwili ikiwemo kichwa cha mtoto kutibuka.

Wanaume hao waliachiliwa na polisi baada ya kuhojiwa Jumamosi kuhusu mikoba iliyopatikana ikiwa na masalia ya binadamu yakiwa yanapelekwa nchini Marekani.

Kwa mujibu wa polisi wafanyakazi wa kampuni ya kusafirisha mizigo ya DHL mjini Bangkok, walikuwa wakifanya shughuli ya kuangalia miizigo iliyokuwa tayari kusafirishwa ikiwa na kibandiko kilichoonyesha mzigo huo ulikuwa na wanasesere.

Walipoufungua na kuangalia ndani ndipo wakagundua kuwa ilikuwa masalia ya sehemu za mwili wa mtoto.

Wanaume hao walifahamisha polisi kwamba masalia yaliyopatikana katika soko moja la usiku na walitaka kuwapa marafiki zao kama zawadi, kwa mzaha tu.

Mmoja wa washukiwa alikuwa mwanamume mmoja mtengeza filamu maarufu. Mikoba hio ilikuwa na kichwa cha mtoto pamoja na mwingine ukawa na mguu uliokuwa umekatwakatwa kwa sehemu tatu.

Pia polisi walipata vipande vya ngozi ya binadamu ikiwa na Tatoo.

Masalia hayo yalipatikana katika mikoba mitano ikiwa na kemikali ya kuyahifadhi. Wafanyakazi wa DHL waliyagundua kupitia kwa mashine ya X-ray.

Akiongea na wandishi wa habari, afisaa mkuu wa polisi alisema kuwa masalia hayo yaliibwa kutoka katika moja ya hospitali kubwa ambayo ipo katika eneo la Thonburi.